Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) yamezihimiza nchi za Afrika kufungua shule na kuhakikisha watoto wanakuwa salama dhidi ya virusi vya corona.
Mashirika hayo yamesema kuendelea kufunga shule kwa muda mrefu kunahatarisha ustawi wa watoto hao ikiwa ni pamoja na kutopata mlo kamili, mimba za utotoni pamoja na aina mbalimbali za uhalifu.
“Lazima tukahikishe kuwa juhudi za kudhibiti virusi vya corona hazitufanyi tuishie kuwa na kikazi kibovu. Kama mbavyo nchi zinafungua biashara kwa usalama, pia tunaweza kufungua shule,” Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Afrika.
Nchi sita pekee kati ya nchi 39 za Afrika ndizo zilizofungua shule kwa mujibu wa takwimu za WHO na UNICEF. Baadhi ya nchi hufungua shule kisha kuzifunga baada ya maambukizi ya corona kuanza kuongezeka, huku nyingine zikifungua kwa ajili ya wanafunzi wanaomaliza au wenye mitihani.
Wakati Tanzania ikiwa imefungua shule katika ngazi zote za masomo, Kenya imefuta mwaka wa masomo 2020, na shule zitafunguliwa mwaka 2021.