Mfumo wetu wa elimu uendane na mabadiliko ya kiteknolojia

0
10

Na Ben Ndunguru, CoET UDSM

Elimu bora kwa kizazi kijacho ni muhimu sana kwa uhai na maendeleo ya nchi.

Hata hivyo katika zama hizi mpya za teknolojia, elimu si tu kumfunisha mtoto namna ya kufanya hesabu na kuandika maneno kwa usahihi, bali ni kuhakikisha kuwa anafahamu namna ya kutumia teknolojia ya kisasa.

Ni muhimu kuwa kizazi cha kesho kikawa na uelewa juu ya kompyuta, jambo litakalowasaidia kufanya shughuli zao kwa kutumia teknolojia hii inayotawala kila kona ya dunia kwa sasa.

Huku serikali ikifanya jitihada kuboresha elimu, ni jema na la faraja kuona sekta binafsi nchini inasaidia kusukuma mbele jitihada hizo kwa kizazi kijacho.

Kwa mfano, siku za hivi karibuni kampuni moja ya mawasiliano nchini Tanzania ilichangia kompyuta 10 zilizounganishwa na huduma ya intaneti bure katika Shule ya Sekondari Kisutu. Inaripotiwa kuwa tayari shule hiyo inatekeleza mkakati wa kuwawezesha watoto wa kike shuleni hapo kutumia vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Kuwafundisha wasichana hao namna ya kutumia teknolojia ya kidijitali, kama vile kutumia kompyuta, kunasaidia kutengeneza fursa kubwa za baadae kama vile kuongeza uwezo wao wa kupata ajira. Kutilia mkazo mfumo huu wa elimu kwa watoto wenye umri mdogo, kunaruhusu kizazi kijacho kuwa na uelewa mkubwa wa teknolojia, kwani teknolojia inazidi kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.

Mkakati huu uliozinduliwa na Kampuni ya Tigo nchini Tanzania unafanya kazi kuhakikisha kuwa kunakuwa na ongezeko la matumizi ya kompyuta.
Hadi sasa, mkakati wa Tigo wa kuhakikisha wanafunzi mashuleni wanajifunza kutumia kompyuta (Tigo e-schools), umeunganisha shule zaidi ya 60, na kampuni hiyo imechangia kompyuta 77 katika taasisi za umma.
Wakati maendeleo ya teknolojia yakizidi kushika kasi, ni muda sahihi mfumo wetu wa elimu nao uendane na mabadiliko hayo.

Faida kubwa itokanayo na jitihada za Tigo katika mkakati huu si tu kunaboresha maisha ya kila siku ya raia wa Tanzania, lakini pia kusaidia kuhakikisha kuwa mfumo wetu wa elimu unabaki salama na wenye tija, wakati tukiendelea katika sekta nyingine kama taifa.

Send this to a friend