Rais wa Yoweri Kaguta Museveni amefanya ziara ya kikazi ya siku 1 hapa nchini ambapo ameungana na Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya kukamilisha majadiliano ya utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Utiaji saini huo umefanyika katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita ambapo marais hao pia wametia saini waraka wa pamoja wa kuagiza kuanza haraka kwa utekelezaji wa mradi huo.
Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt. Medard Kalemani amesema bomba litakalojengwa litakuwa na urefu wa kilometa 1,445 ambapo kilometa 1,149 kati yake zinapita nchini Tanzania, litapita katika mikoa 8, wilaya 24 na vijiji 280 hapa nchini, litakuwa na uwezo wa kupitisha mapipa 216,000 kwa siku, litazalisha ajira 10,000 na kwamba kwa miaka 25 ya mradi huo Tanzania itapata mapato ya kiasi cha shilingi Trilioni 7.5.
Rais Magufuli amempongeza na kumshukuru Rais Museveni kwa kuchukua hatua madhubuti za kutafuta mafuta nchini mwake, kukubali bomba lipitishwe nchini Tanzania na pia kuridhia asilimia 60 ya faida ichukuliwe na Tanzania (ambako bomba linapita kwa Zaidi ya asilimia 70) ilihali Uganda ikichukua faida kwa asilimia 40.
Aidha, Rais Magufuli ameeleza kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutarahisisha upelekaji wa gesi ya Tanzania nchini Uganda kupitia njia hiyo hiyo na pia kutarahisisha usafirishaji wa mafuta yanayotafutwa katika mbuga ya Wembele nchini Tanzania.
Kwa upande wake Rais Museveni amesema utafiti uliofanywa katika asilimia 40 ya bonde la mto Albert huko Hoima nchini Uganda umebaini kuwepo kwa mapipa bilioni 6.5 ya mafuta ghafi na kwamba zipo dalili njema kuwa asilimia 60 za eneo ambalo halijatafitiwa pia kuna mafuta na kwamba Uganda inatarajia kupata mafuta mengine katika ukanda wa Kadamu.
Rais Museveni amerejea nchini Uganda.