Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Hayati Mark Bomani amezikwa leo katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Jaji Bomani alizaliwa Januari 2, 1932 na alikuwa kati ya watoto 10 wa Mzee Bomani. Alisoma shule ya msingi Mwamanyili, Nassa ambapo baba yake mzazi ndiye alikuwa mwalimu wake. Alipomaliza shule ya msingi alijiunga na Shule ya Wavulana ya Bwiru ambapo alisoma hadi darasa la 10.
Alifaulu na kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora na ambako pia alifaulu na kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere cha nchini Uganda mwaka 1953 hadi 1957 ambako alipata Shahada ya Kwanza ya masuala ya Siasa, Uchumi na Historia. Mwaka 1957 hadi 1958 alijunga na Taasisi ya Ustawi wa Jamii ya The Hague na alitunukiwa diploma ya masuala ya jamii.
Mwaka 1958 hadi 1961 alijiunga na chuo Kikuu cha London nchini Uingereza na kutunukiwa shahada ya kwanza ya sheria.
Mwaka jana aliugua na kupata matibabu nchini Afrika Kusini na India, hali yake ilikuwa nzuri na aliweza kurejea katika kazi alizozipenda za sheria lakini hali yake ilibadilika ghafla na alifariki dunia Septemba 10, 2020 na ameacha mke, watoto watatu na wajukuu sita.
Katika mazishi hayo, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wamuenzi Jaji Mstaafu, Hayati Mark Bomani kwa kuuishi utumishi wake uliotukuka aliouonesha wakati wa kipindi chote cha uhai wake.
Majaliwa ametoa wito huo leo alipoongoza waombolezaji kuuaga mwili wa kiongozi huyo aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, shughuli iliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee na kufuatiwa na mazishi kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Wote sisi ni mashahidi wa mchango mkubwa wa mzee wetu alioutoa katika tasnia ya sheria na katika nafasi mbalimbali alizotumikia ndani na nje ya Tanzania,” amesema Waziri Mkuu.
Bomani aliteuliwa kushika nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 1965 hadi 1976, nafasi ambayo aliitumikia kwa uaminifu, uadilifu na umahiri mkubwa na alifanikiwa kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha sekta ya sharia inaimarika, amesisitiza Majaliwa.