App Inc na serikali ya Singapore zimeingia makubaliano ya kushirikiana kwa miaka miwili katika mradi wa kiafya unaofahamika kama LumiHealth ambapo utakuwa unafuatilia na kutoa zawadi kulingana na tabia za matumiaji kwa kutumia saa za Apple (Watch) pamoja na programu tumishi ya iPhone.
Kupitia mpango huo raia wa Singapore wataweza kujishindia hadi $280 (takribani TZS 650,000) kama zawadi au vocha kwa kufikia lengo lililowekwa katika programu. Lengo hilo linaweza kufikiwa kwa kuogelea, kutembea au yoga, na programu ya LumiHealth itatoa maelezo kwa mtumiaji namna ya kufanya mazoezi na muda wa kufanya uchunguzi wa afya.
Mpango huo unaelezwa kuwa utawafanya watu wengi kubadili mifumo yao ya maisha ikiwa ni pamoja na kuongeza ari ya mazoezi, kuzingatia chakula na kulala kwa muda wa kutosha.
Programu ya LumiHealth inaelezwa kuwa ni salama kwani inazingatia usiri wa taarifa za mtumiaji na Apple imesema kuwa hakuna taarifa itakayouzwa kwa lengo la kibiashara.
Naibu Waziri Mkuu wa Singapore, Heng Swee Keat amesema kuwa licha ya kwamba dunia inaendelea kukabiliana na janga la corona, ni lazima watu wawekeze kwenye maisha ya mbeleni na hakuna njia bora ya kuwekeza kama kuwekeza kwenye afya ya mtu mmoja mmoja.