Ufafanuzi wa NEC kuhusu adhabu aliyopewa Tundu Lissu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa haijatoa adhabu kwa mgombea Urais wa Tanzania kupitia CHADEMA, Tundu Lissu bali adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Maadili ya Kitaifa.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa kamati hiyo, Emmanuel Kawishe imeeleza kuwa kumekuwa na tafsiri isiyokuwa sahihi kuhusu adhabu hiyo ambapo baadhi ya watu wanaamini umma wa Watanzania kwamba mgombea huyo ameadhibiwa na NEC.
“Lissu ameadhibiwa na kamati ambayo inajumuisha wawakilishi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi wa kiti cha Rais. “Kamati si Tume ya Taifa ya Uchaguzi, bali ni chombo kinachoundwa na vyama vyote vyenye wagombea wa kiti cha Rais kikiwemo CHADEMA,” imeeleza taarifa hiyo.
Kawishe ametoa ufafanuzi zaidi na kueleza kuwa mbali na wajumbe kutoka vyama 15 vyenye wagombea Urais, kamati hiyo pia inaundwa mjumbe mmoja kutoka serikalini na mjumbe wa NEC ambaye ndiye mwenyekiti.
Kuhusu madai ya Lissu kuwa hakupata nafasi ya kujitetea, Kawishe ameeleza kuwa katika kikao cha kamati kulikuwa na mawakili wawili kutoka CHADEMA waliosimama kutetea hoja za Lissu.
Mgombea huyo amepewa adhabu ya kutofanya kampeni kwa muda wa siku saba kuanzia Oktoba 3 mwaka huu, na kwamba hatoruhusiwa kuendelea na kampeni zake au kwa ajili ya mgombea mwingine.