Rais wa Malawi: Tufanye chaguzi bila waangalizi wa nje
Zikiwa zimebaki siku 20 kufanyika uchaguzi mkuu nchini Tanzania, Rais wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera amesema ni muhimu Afrika ikafanya chaguzi zake bila kuwa na waangalizi wa kimataifa.
Dkt. Chakwera amesema hayo katika Ikulu ya Tanzania (Dar es Salaam) wakati wa mkutano na waandishi wa habari ambapo ameongeza kuwa waangalizi hao wanapokuja Afrika huandika habari wanazotaka wao.
“… tuweze kufanya chaguzi zetu bila kuwa na hao waangalizi wa kimataifa, kwa sababu wanapokuja hutoa taarifa wanazoamua wenyewe. Kwa hiyo tunaamini kuwa Afrika inaweza kuimarisha demokrasia yake yenyewe.”
Amesema kuwa badala ya kutegemea usaidizi wa nje, ni muhimu nchi za Afrika zikasimamia taasisi zake zenyewe na isimulie mambo yake yenyewe.
“Ni sisi wenyewe kuchukua jukumu letu na sio mtu mwingine.”
Kwa upande wa biashara, Rais Chakwera na Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli wamefikia makubaliano mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha pamoja cha forodha na wizara inayoshughulikia uchukuzi ya Tanzania ifungue ofisi mjini Lilongwe ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo.
Viongozi hao wamekubaliana pia kuwa maafisa kutoka mchi hizo watajengeana uwezo katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini ambayo kwa upande wa Tanzania imekuwa ikiimarika.
Rais Chakwera amewasili nchini Tanzania leo kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu ambapo atatembelea Bandari ya Dar es Salaam na kuweka jiwe la msingi kwenye kituo kipya cha mabasi ya mikoani, Mbezi Mwisho.