Sekta ya mawasiliano ya simu na kukua kwa teknolojia kunavyobeba fursa za uwekezaji nchini
Emilian Kitine, DIT
Hakuna shaka yoyote kwamba mapinduzi ya kiteknolojia yameleta mabadiliko makubwa katika maisha yetu ya kila siku.
Ugunduzi wa kupata mtandao wa intaneti ni moja ya mabadiliko makubwa zaidi katika teknolojia, kwamba leo hii ukiwa na simu janja yako na bando basi unapata intaneti. Programu tumishi, kwa Kiingereza Apps sasa zimekuwa sehemu muhimu kabisa ya maisha yetu na hakika zimekuja na fursa mbalimbali.
Intaneti kwa njia ya simu imewezesha hata watu kufanya biashara wakiwa maeneo tofauti ndani na nje ya nchi na pia kuzitangaza biashara zenyewe kwa watu mbalimbali mitandaoni. Bila teknolojia hii, hakika ingekuwa ngumu kwa wauzaji na wanunuzi kuwasiliana na pia kutangaza biashara hizi.
Huduma ya intaneti pia imesaidia mawasiliano murua kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter na Instagram. Sasa unabofya tu kidude na uko hewani tayari unawasiliana iwe kwa sauti ama video.
Kutokana na maendeleo haya ya kasi kwenye teknolojia, usambaaji wa intaneti umeongezeka maradufu kati ya mwaka 2013 hadi 2019. Hii inaashiria kuwa kusambaa kwake kutakua zaidi katika miaka inayokuja.
Kuzidi kusambaa kwa kasi kwa matumizi ya huduma za intaneti nchini kumezifanya kampuni za mawasiliano za Tanzania kuwekeza katika huduma ambazo zina tija kubwa sana kwa wateja wake.
Mfano, Tigo Tanzania imekuwa moja ya watoa huduma wakubwa zaidi nchini na imejidhatiti kupanua wigo zaidi linapokuja suala la kuleta ufumbuzi wa kibunifu kwenye teknolojia kwa ajili ya wateja wake.
Mifano ya karibuni ni pamoja na huduma ya kuongeza muda wa maongezi kwenye simu, Tigo Rusha. Huduma hii inawaruhusu wateja kujiunga na vifurushi mbalimbali kielektroniki pasi na kuwa na haja ya kununua vocha za kukwangua. Hii ni njema hata kwa mazingira kwani sasa hakuna tena kuchafua na zile vocha baada ya kukwangua, unajaza kidijitali.
Pia, Tigo inashirikiana na ZanFast Ferries ambapo abiria wanaweza kukata tiketi ya safari kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kutumia Tigo Pesa.
Kutokana na hilo, ni muhimu watoa huduma za mawasiliano ya simu wakapata ushirikiano kutoka kwa mamlaka husika, ushirikiano ambao utaziwezesha kampuni kama Tigo kubaki imara katika soko na kuendelea kusaidia wananchi kufaidi huduma zake na fursa zinazotokana na huduma hizo. Vile vile katika kuendelea mbele ni muhimu wadau wote wakashirikiana kwa karibu na sekta hii kuhakikisha kuwa mahitaji yake ya kukua zaidi kiuwekezaji yanapatikana, jambo ambalo litachochea uwekezaji zaidi na ukuaji wa teknolojia.
Kwa kufanikisha hili, si tu litawasaidia wateja, lakini watu wote ambao wamekuwa wakinufaika na huduma za intaneti pamoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.