Serikali ya Rwanda imeidhinisha kilimo cha bangi kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi, lakini matumizi yake ndani ya nchi yameendelea kupigwa marufuku.
Kwa hatua hiyo serikali inalenga kuongeza mapato yatokanayo na kusafirisha bidhaa nje ya nchi ambapo soko la bangi duniani linatajwa kuwa na thamani ya $345 bilioni (TZS trilioni 800).
Uamuzi huo umeibua mjadala nchini humo ambapo baadhi ya waliotoa maoni yao wamesema fursa hiyo inaweza ikachochea matumizi ya dawa hiyo ya kulevya endapo hatua kali za kudhibiti hazitochukuliwa.
“Hii haitotoa mwanya kwa watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya. Sheria dhidi ya dawa za kulevya ipo na itaendelea kutekelezwa,” amesema Waziri wa Afya wa Rwanda, Dkt. Daniel Ngamije.
Baraza la mawaziri nchini humo likiongozwa na Rais Paul Kagame Jumatatu Oktoba 12 lilipitisha kanuni za muongozo wa kulima, kuchakata na kusafirisha nje ya nchi bidhaa hiyo kwa ajili ya matibabu.