ACT-Wazalendo ‘yamruka’ Bernard Membe
Chama cha ACT-Wazalendo kimeeleza kusikitishwa na kauli zilizotolewa na mgombea Urais wa chama hicho, Bernard Membe jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa yeye ni mgombea halali wa chama hicho.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Seif Sharif Hamad wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mchakato wa kampeni na suala la kupiga kura, ambapo amesema wanaamini wataing’oa CCM bara na visiwani.
Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua msimamo wa ACT-Wazalendo kuhusu aliyoyasema Membe, mwanasiasa huyo mkongwe amesema uongozi wa chama ulikubaliana, na membe akiwepo, wamuunge mkono mgombea Urais wa CHADEMA, Tundu Lissu.
“Nasikitika sana kwa aliyoyazungumza Membe jana. ACT-Wazalendo kupitia mkutano mkuu wa Taifa tuliamua tunataka mabadiliko katika nchi yetu. Mkutano mkuu ukabariki tushirikiane na vyama makini kuiondoa CCM madarakani.
Membe alipokuja tulimwambia maamuzi ya mkutano mkuu ni tushirikiane na vyama vingine. Tukamuuliza tukiamua kushirikiana utakubali, akasema “Naam.” Tulipoona kampeni zetu zimesuasua, tukaamua, na Membe akiwepo, tumuunge mkono Lissu.”
Amemshutumiwa Membe kwamba huenda alijiunga na chama hicho cha upinzani ili kukivuruga kisiweze kuiondoa CCM madarakani.
“Hakuna mpasuko ndani ya ACT-Wazalendo. Membe anataka iaminike hivyo, lakini hakuna. Chama kimefanya uamuzi, wewe unaenda kinyume. Tukuelewe vipi? Si umeletwa ACT kwa mission (shughuli) maalum,” amesema Hamad ambaye pia ni mgombea Urais Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo
Aidha, amesema kuwa chama hicho kiliamua kumuunga mkono Lissu kwa sababu ndiye mgombea anayeonekana kwamba anaweza kuishinda CCM. Pia, ametoa angalizo kuwa, kumuunga mkono Lissu hakumaanishi kwamba chama hicho kinawaunga mkono wagombea wa CHADEMA katika ngazi zote.
Kabla ya kuzungumza haya, Maalim Seif alieleza mambo kadhaa ambayo yanatia mashaka mchakato wa uchaguzi visiwani Zanzibar, huku akiihimiza Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kurekebisha kasoro hizo ili uchaguzi uwe huru na wa haki na Wanzanzibari wapate viongozi wanaowataka.