Jitihada za chama tawala cha Zambia za kupitisha muswada wa mabadiliko ya Katiba ambayo yangemuongezea nguvu/mamlaka Rais wa nchi hiyo zimekwama.
Chama hicho kilikusudia kumpa Rais Edgar Lungu mamlaka zaidi juu ya mfumo wa uchaguzi, mamlaka juu ya sera za kifedha za benki kuu ya nchi hiyo na kupunguza mamlaka ya bunge katika kuisimamia serikali.
Mabadiliko hayo yanayofahamika kama Muswada Namba 10 hayakupita baada ya kushindwa kupata kura zilizohitajika ambazo ni mbili ya tatu ya kura zote. Muswada ulipata kura 105 na zilizohitajika ni 111.
Baadhi ha wananchi na wanasiasa wa upinzani nchini humo wamefurahia kukwama kwa muswada huo ambao wamesema kuwa una malengo binafsi kwa viongozi na si maslahi ya umma.