Godbless Lema akamatwa Kenya akitafuta hifadhi Ubalozi wa Marekani

0
11

Aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini kupitia CHADEMA, Godbless Lema amekamatwa na Polisi katika Kaunti ya Kajiando nchini Kenya baada ya yeye na familia yake kuvuka mpanga wa Namanga.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Standarnd Media ya Kenya Lema alikuwa na mkewe, Neema Godbless na watoto wao watatu.

Lema ameliambia gazeti hilo kuwa maafisa wa uhamiaji walikataa kugonga muhuri nyaraka zilizowasilishwa na mke wake, kwa madai hadi wamuone Lema. Amesema mke wake alipomuita alikwenda lakini akawaambia hana hati yake ya kusafiria kwa sababu alikuwa hasafiri, na kwamba mke na wanae walikuwa wanakwenda kutafuta shule ya kimataifa Kenya.

Maafisa waliruhusu mke na watoto kuvuka mpaka, na Lema aliomba kwenda kutafuta fedha za Kenya ili ampe mke wake ambaye alisema kwamba angeendelea na safari yeye na watoto.

Lakini mara tu alipovuka mpaka, Lema na familia yake waliingia ndani ya gari la mwanasheria wake, George Luchiri ambaye alikuwa akifuatilia mchakato mzima wa Lema kuvuka mpaka kuingia Kenya.

Maafisa hao wa uhamiaji walitoa taarifa polisi kwamba kuna mtu ameingia nchini humo pasi na kuwa na nyaraka husika.

“Polisi walitufuatilia na wakatukamata tukiwa Ilbisil na kutupeleka kwenye kituo cha polisi. Sikutaka wamuweke Lema hapo kutokana na ukaribu wake na mpaka wa Tanzania,” mwanasheria huyo ameiambiba The Standard Media.

Mwanasheria huyo amesema alifahamu kwamba Lema anakwenda Kenya na kwamba alitaka ampeleke Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNHCR) mara tu atakapavuka mpaka.

Luchiri amesema kwa mujibu wa UNHCR mtu anayetafuta hifadhi hahitaji kuwa na nyaraka za kumuwezesha kuingia nchi nyingine.

Akieleza sababu za kutokutoa hati yake ya kusafiria, Lema amesema alijua kwa kufanya hivyo, maafisa hao wangemshikilia na kumzuia kuvuka.

“Nimeacha kila kitu nyumbani. Hivyo havina umuhimu kwa sasa. Muhimu  ni usalama wangu na usalama wa familia yangu. Nipo na wanangu Allbless, Brilliance na Terrence. Sijui kesho itakuja na nini. Kwa sasa natafuta hifadhi,” Lema ameiambia The Standard.

Mwanasheria huyo amesema atawasilisha taarifa za Lema katika Ubalozi wa Marekani kwani amekuwa akifanya mawasiliano na maafisa wa ubalozi huo.

Wakati hilo likitokea, aliyekuwa mgombea Urais wa Tanzania kupitia CHADEMA, Tundu Lissu yupo Ubalozi wa Ujerumani jijini Dar es Salaam alipokwenda kuomba hifadhi akidai ametishiwa kuuawa.

Send this to a friend