Tanzania yatoa rai kwa Jumuiya ya Kimataifa kutatua matatizo ya Afrika
Tanzania imetoa rai kwa Jumuiya ya Kimataifa na Japan kuendelea kutafuta suluhu ya kudumu kwenye changamoto mbalimbalii ambazo bado zinajitokeza kwenye baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo ugaidi wa kimataifa, uhalifu, mabadiliko ya tabianchi, ukame, njaa na magonjwa sambamba na kujitolea kuchangia na kuwekeza kwenye miradi iliyobuniwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuboresha mazingira yaliyoharibiwa kutokana na uwepo wa kambi za Wakimbizi kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Rai hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu kuimarisha amani na usalama barani Afrika uliofanyika wakati wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliomalizika leo tarehe 30 Agosti 2019 jijiji Yokohama, Japan.
Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa, miradi hiyo ambayo ni pamoja na kubadilishana teknolojia hususan kwenye maeneo ya mipakani na mifumo ya kutoa taarifa mapema kwa ajili ya kujikinga na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza itasaidia kuboresha mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yameharibiwa na wakimbizi na watu wanaotafuta makazi.
“Uwepo wa wakimbizi na watu wanaotafuta makazi kwa namna moja au nyingine huathiri mazingira, jamii usalama na uchumi wan chi inayowapokea. Hivyo ni ombi letu kwenu kushirikiana nasi kwenye miradi mbalimbali katika kuboresha mazingira” alisema Mhe. Waziri Mkuu.
Aliongeza kusema kuwa, kwa miaka mingi Tanzania imekuwa kimbilio kwa wakimbizi kutoka nchi jirani wanaokimbia nchi zao kutokana na migogoro ya kisisasa, kikabila na kuibuka kwa vikundi vya uasi. Alieleza kuwa hadi kufikia tarehe 1 Agosti 2019, Tanzania inahifadhi wakimbizi wapatao 305,983.
Vilevile, Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kuwa, katika kuhakikisha amani inapatikana pote dunaiani, Tanzania ina mchango mkubwa katika amani, utulivu na utatuzi wa migogoro barani Afrika na kwamba ni miongoni mwa nchi zinazochangia misheni za ulinzi wa amani katika nchini mbalimbali Afrika na duniani.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mkuu amefanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Bw. Fillipo Grandi walipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Saba wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika.
Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Waziri Mkuu na Bw. Grandi wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kuhakikisha usalama kwenye makambi ya wakimbizi, kuimarisha mipaka pamoja na kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na Wakimbizi.
Akizungumzia Mkutano wa Saba wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliofanyika kwa siku tatu jijini Yokohama, Japan. Mhe. Waziri Mkuu amesema Mkutano huo umemalizika kwa mafanikio huku Wakuu wa Nchi a Serikali wakikubaliana kuteleleza Azimio la Yokohama linalolenga kuleta mapinduzi barani Afrika kwa kuimarisha masuala ya usalama, elimu, sayansi na teknolojia na kukuza sekta binafsi.
Amesema kuwa, Tanzania itajipanga kikamilifu kutekeleza maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano huo ambayo ni ya manufaa makubwa kwa nchi za Afrika.
Mhe. Waziri Mkuu alieleza kuwa, maazimio hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamegusa sekta zote muhimu zikiwemo afya, elimu, maendeleo ya miundombinu, sayansi na teknolojia na amani na usalama yanalenga kuzikwamua kiuchumi nchi za Afrika kupitia ushirikiano na Serikali ya Japan.
“Tumemaliza kikao cha TICAD leo ambacho kimejadili mambo mengi yakiwemo ya usalama, maendeleo ya elimu, sayansi na teknolojia na namna nzuri ya kuendesha nchi zetu kupitia miradi ya maendeleo kama ujenzi wa miundombinu. Kikao hiki kwetu Tanzania ni chachu ya kuendeleza jitihada zetu za kufikia uchumi wa kati na mapinduzi ya viwanda ifikapo mwaka 2025” alifafanua Waziri Mkuu.
Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kuwa, Japan imetenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi za Afrika kupitia fursa ya mikopo na ufadhili. Aliongeza kuwa, Tanzania itajipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kuandaa maandiko mazuri ya miradi ya kipaumbele ili kupata fedha hizo.
Amesema kuwa, nchi za Afrika ambazo kwa kiasi kikubwa zimejaliwa kuwa na maliasili na malighafi za kutosha kwa ajili ya kujenga uchumi, zimesisitizwa kuimarisha mahusiano na sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa nchi hizo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan
30 Agosti 2019