Francisco Sagasti ameapishwa kuwa Rais wa muda wa Peru, akiwa ni Rais wa tatu kuliongoza Taifa hilo la Amerika ya Kusini ndani ya wiki moja.
Sagasti mwenye umri wa miaka 76 anatarajiwa kuliongoza Taifa hilo linaloandwamwa na misukosuko ya kisiasa hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika mwakani.
Mhandisi huyo aliyegeukia siasa ametwaa nafasi hiyo kutoka kwa Rais wa muda na aliyekuwa Spika wa Bunge la Juu (congress) la nchi hiyo, Manuel Merino ambaye alishika wadhifa huo tangu wiki iliyopita kufuatia kuong’olewa madarakani kwa Rais Martín Vizcarra.
Maelfu ya wananchi nchini humo wameandamana kushinikiza Merino ajiuzulu kutokana na kutumia nguvu kakukabiliana na waandamanaji waliokuwa wakipinga Rais Vizcarra kuondolewa kwenye nafasi hiyo.
Rais Vizcarra aliondolewa madarakani (imleached) kutokana na tuhuma za rushwa ambazo amekanusha.
Akilihutubia bunge, Rais Sagasti ameomba msamaha kufuatia vifo vya wale waliouawa kwenye maandamano, na amewataka wananchi kuwa watulivu kwani hawawezi kurejesha maisha ya wale waliouawa.
Amesema moja ya kazi zake kubwa ni kuhakikisha uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyka Aprili 2021 unakuwepo.