Mkurugenzi wa Mashitaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga amesema wanaolalamika kuwa amemfutia kesi kada wa CHADEMA, Nusrat Hanje isivyo sahihi wanakiuka utaratibu .
Maganga amesema hayo mkoani Kilimanjaro wakati akitoa ufafanuzi kuhusu kufutwa kwa mashitaka dhidi ya kada huyo aliyefukuzwa uanachama wa CHADEMA hivi karibuni na kusema kuwa alifuta mashitaka hayo kwa mamlaka aliyonayo kisheria chini ya kifungu cha 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
DPP ameeleza kuwa sheria za nchi zipo na zinafanya kazi kwa wananchi wote bila upendeleo.
DPP amesema hayo baada ya baadhi ya watu kuhoji ni kwa namna gani Bi. Hanje ameweza kutoka gerezani na kuapishwa kuwa mbunge wa viti maalum.
Kabla ya Maganga, Halima Mdee jana Disemba 1, 2020 aliwaambia waandishi wa habari kuwa Bi. Hanje aliweza kuapishwa kuwa mbunge wa viti maalum kwa sababu alishiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 akiwa kama mgombea.
Bi. Hanje alivuliwa uanachama wa chama hicho na wenzake 18 mara baada ya kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum hatua iliyotafsiriwa na chama kuwa ni ukiukwaji wa taratibu na sheria.
Kamati Kuu ya CHADEMA ilifikia uamuzi huo kwa kile ilichoeleza kuwa haijateua wabunge wa viti maalum.