China imesema itaangalia namna ya kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway) na bwawa la kuzalisha megawati 2,115 za umeme katika mto Rufiji (Bwawa la Mwl. Nyerere)
Hayo yamesemwa leo Disemba 15, 2020 na Rais wa China, Xi Jinping alipompigia simu Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli ambapo viongozi hao wamezungumzia kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano hususani katika masuala ya uchumi.
Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa muda wa saa moja, Rais Xi Jinping amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa tena na kwamba anaiona Tanzania kuwa nchi itakayoongoza kwa ukuaji wa uchumi barani Afrika.
Kwa upande wake Rais Magufuli amemhakikishia Rais Xi Jinping kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na China uliodumu kwa takribani miaka 55 baada ya kuasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong, na kwamba Tanzania itaendelea kuiunga mkono China katika masuala mbalimbali ya kimataifa.
Rais Magufuli ameiomba China kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji wa miradi mikubwa kwa kutoa mikopo nafuu na ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni wa kuzalisha megawati 358 za umeme katika mto Ruhudji, Megawati 222 za umeme katika mto Rumakali na ujenzi wa barabara visiwani Zanzibar.
Halikadhalika, Dkt. Magufuli ameiomba China kufungua zaidi masoko ya bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania hususani mazao mbalimbali ya kilimo.
Rais Xi Jinping ameahidi kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na Rais Magufuli ikiwemo ujenzi wa miradi ya kuzalisha umeme ya Ruhudji na Rumakali, ujenzi wa reli, Bwawa la Nyerere na ununuzi wa mazao ya Tanzania.