Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini kutokuwa kikwazo katika utoaji wa vibali vya mazingira kwa wawekezaji katika kutekeleza miradi ya kimkakati.
Amesema hayo hii leo alipokuwa akizungumza na Menejimenti na wafanyakazi wa NEMC mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika ofisi za NEMC mikocheni jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi yanayotolewa na wawekezaji ndani ya nchi juu ya utoaji wa vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira ambavyo taratibu zake zinachukua muda mrefu na kusababisha ucheleweshwaji wa maendeleo katika nchi yetu na kuleta usumbufu usio wa lazima kwa wawekezaji.
“Katika hili nimewaagiza NEMC kuharakisha mchakato wa kutoa vibali vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa wakati. Hata hivyo nimebaini kwamba ucheleweshwaji wa vibali hivyo kwa kiasi kikubwa hausababishwi na NEMC bali changamoto kubwa iko kwa wale washauri elekezi ambao ndio wanafanya hizo Tathmini za Athari kwa Mazingira. Kuna haja kubwa kuwasimamia washauri elekezi wa mazingira ambao sio waaminifu. Katika kusimamia hilo tutahakikisha tunaunda kanuni mpya ambazo zitasimamia wataalamu hao,” amesema Ummy.
Kuhusu biashara ya chuma chakavu, ametoa muda wa siku 14 kwa Baraza kukutana na taasisi nyingine zinazohusika na biashara hiyo ili kuwa na muongozo bora wa kulinda miundombinu ya umma.
“Tutakuwa makini zaidi, kuhakikisha biashara ya vyuma chakavu inasimamiwa kikamilifu ili kufikia azma ya Rais Dkt. Magufuli, hatutaki biashara hii kuhujumu miundombinu ya Serikali, tutakuwa makini zaidi kuhakikisha vyuma chakavu having’olewi kutoka kwenye mataruma ya reli, alama za barabarani au madaraja.”
Kuhusu utunzaji mazingira amesema “Tumeainisha maeneo makubwa manne ambayo tutayafanyia kazi ili kutunza mazingira. Maeneo hayo ni Viwanda, Migodi, Ujenzi holela katika vyanzo vya maji, pamoja na usimamizi madhubuti wa biashara ya vyuma chakavu.”