Jukumu la kampuni za simu katika kuwajengea Watanzania ujuzi wa kidijitali
Rufina Ndekao, DIT
Inafahamika wazi kuwa teknolojia imebadili maisha ya binadamu na mabadiliko mengi zaidi bado yanaendelea kuja. Tanzania ni moja ya nchi ambamo maendeleo ya kiteknolojia yanazidi kuonekana yakibadili maisha ya watu siku hadi siku, mfano kuongezeka kwa matumizi ya mtandao wa intaneti. Ukitazama takwimu, mwaka 2013 matumizi ya intaneti Tanzania yalikuwa asilimia 20 tu, lakini hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2019 yalikuwa yamefikia asilimia 46.
Utafiti wa Benki ya Dunia unaonesha kwamba, siku zijazo karibu kila kazi duniani itahitaji aina fulani ya ujuzi wa teknolojia ya kidijitali. Huu ni ukweli usiopingika unamaanisha kuwa ni muhimu sana kuhakikisha wananchi wanajengewa uwezo wa ujuzi wa kidijitali ili kuwa washindani katika kazi.
Ili kufanikisha jambo hili la kujengea Watanzania uwezo wa kidijitali ni muhimu kwamba shule na taasisi nyingine za elimu ziendelee kutengeneza mitaala ambayo inazingatia kuwapa wahitimu ujuzi wa teknolojia ya kidijitali. Huku msambao wa intaneti ukiongezeka na asilimia kubwa ya Watanzania wakiwa ni vijana, Tanzania iko katika nafasi muhimu ya kufanikiwa kwenye uchumi wa kidijitali.
Ni muhimu kukumbuka kwamba maendeleo haya ya kidijitali nchini Tanzania yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na sekta binafsi.
Mfano mmojawapo wa wadau katika sekta hii ni Tigo Tanzania, moja ya kampuni kubwa za mawasiliano ya simu. Tigo imeingia ubia na mradi wa Apps and Girls katika kuhakikisha kwamba watoto wa kike na wanawake kwa ujumla wanapata ujuzi kwenye mambo ya teknolojia.
Tigo pia imetoa msaada wa kompyuta na uunganishaji na mtandao wa kwa shule mbalimbali za sekondari nchini ili kuwajenga wanafunzi ujuzi katika kazi zao baada ya masomo.
Mambo haya na mengine yanaonesha umuhimu wa sekta binafsi katika kujengea Watanzania uwezo na ujuzi wa kidijitali.
Jinsi ambavyo teknolojia inaendelea kukua, tuendelee kuenzi mchango wa sekta binafsi katika maendeleo haya na kuijengea mazingira ya kukua na kutoa mchango mkubwa zaidi na zaidi.