Kanisa lamtunuku Rais Dkt. Magufuli Tuzo ya Uongozi Bora

0
12

Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly limemtunukia Tuzo ya Uongozi Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wake.

Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa la hilo, Dkt. Yohana Masinga iliyofanyika mkoani Dodoma.

Baada ya kupokea tuzo hiyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na Rais mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu na katika hotuba na maelekezo yake kwa viongozi na watendaji wa Serikali amekuwa akisisitiza suala la kumtanguliza Mungu mbele katika kuwahudumia wananchi.

“Ama kwa hakika hofu ya Mungu aliyonayo kiongozi wetu ndiyo hasa siri ya kufanikiwa kwa uongozi wake na Taifa letu kwa ujumla. Sote ni mashuhuda kwamba Tanzania chini ya uongozi wake imekuwa nchi ya mfano Afrika na Dunia kwa ujumla katika kupiga vita rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma sambamba na kurejesha nidhamu ya kazi ambayo ilikuwa imepotea katika ofisi za umma.”

Ametumia fursa hiyo kuwahakikishia kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango wa madhehebu ya dini katika kujenga mustakabali wa sasa na wa baadaye wa nchi yetu. Kadhalika, Serikali inathamini mchango wa madhehebu ya dini katika kutoa huduma za jamii hususan elimu, afya, maji na makundi maalum yenye uhitaji wakiwemo yatima, wajane na wengineo.

Kwa upande wake, Askofu Masinga amesema kanisa limetoa tuzo ya utumishi uliotukuka kwa Rais Dkt. Magufuli baada ya kutambua kazi njema na bora ambayo imefanyika chini ya uongozi wake uliojaa hekima, umakini, ujasiri bila ya kuyumbishwa na watu na hivyo kuliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kati kabla ya wakati uliotarajiwa.

“Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly na uongozi wake tumeona na kutambua kazi njema na bora ambayo imefanyika chini ya uongozi wako, ikiwa ni pamoja na kulinda rasilimali za Taifa kama madini yetu, hifadhi za Taifa na kuwakumbuka wanyonge ukisisitiza wapewe haki zao. Tunakuombea Baraka afya njema wewe na familia yako.”

Send this to a friend