Tanzania kuomboleza kifo cha Rais Mugabe kwa siku 3

0
12

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza siku 3 za maombolezo ya Kitaifa kufuatia kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe Ndg. Robert Gabriel Mugabe kilichotokea leo tarehe 06 Septemba, 2019 nchini Singapore alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika siku 3 za maombolezo zinazoanzia leo 06 Septemba, 2019 hadi 08 Septemba, 2019 bendera zitapepea nusu mlingoti.

Leo asubuhi, Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa, familia ya Mzee Robert Gabriel Mugabe, wananchi wa Zimbabwe, Waafrika na wote walioguswa na musiba huu.

Katika salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amesema “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe Mzee Robert Gabriel Mugabe. Afrika imepoteza mmoja wa viongozi jasiri, shupavu, mwanamajumui wa Afrika (Pan-Africanist) na aliyekataa ukoloni kwa vitendo, Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.”

Rais Magufuli ameongeza kuwa Hayati Robert Gabriel Mugabe aliipenda Tanzania, alijenga uhusiano na ushirikiano wa karibu, kidugu na kirafiki na Tanzania tangu enzi za uongozi wa Baba wa Taifa la Tanzania Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kwamba Afrika itamkumbuka kwa jinsi alivyoshirikiana na viongozi mbalimbali kupinga ukoloni na ukandamizaji wa haki za Waafrika.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Septemba, 2019

Send this to a friend