Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kutengeneza kanzi data ya wataalamu wake walioshiriki ujenzi wa madaraja yote makubwa nchini.
Amesema hatua hiyo itawezesha kuwashirikikisha mara kwa mara watalaamu hao ili kupata ujuzi na uzoefu wa kutosha wa kazi hizo hivyo kuliwezesha Taifa kuwa na hazina ya wataalamu wa ujenzi wa madaraja makubwa watakao simamia ukarabati wake pamoja na kujenga mapya siku za usoni.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa Daraja la Tanzanite Waziri Mkuu amepongeza hatua iliyofikiwa na kuwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili daraja hilo likamilike kwa wakati.
“Kazi yenu ni nzuri hakikisheni daraja hili linakamilika kwa wakati, ili watanzania waweze kunufaika na hivyo kuongeza fursa za utalii hapa nchini,” amesema Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa ameutaka uongozi wa Manispaa ya Jiji la Dar es salaam kuhakikisha sehemu barabara iliyobaki yenye urefu wa kilometa tatu nje ya mradi huo inajengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri katika ukanda huo wa fukwe ya Bahari ya Hindi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa mradi wa ujenzi wa Daraja la Tanzanite utakamilika kwa wakati.
Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo umetoa fursa za ajira za moja kwa moja kwa watanzania zaidi ya 500 na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mradi wa ujenzi wa Daraja la Tanzanite unahusisha daraja lenye urefu wa 1.03km pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa 5.02km unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba 2021.