Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli ameitaka Sekretarieti ya Maadili ya viongozi kuachana na ujazaji na uwasilishaji wa fomu za maadili ya uongozi kwa njia ya mtandao ili kuepusha uvujaji wa siri na ubadilishaji wa maudhui ya fomu hizo, na badala yake fomu zichukuliwe mtandaoni na kisha kujazwa na kuwasilishwa nakala halisi kwa ofisi husika.
Dkt. Magufuli amesema hayo leo Disemba 24, 2020 wakati akimuapisha Sivangilwa Mwangesi (Jaji wa Mahakama ya Rufani) kuwa Kamishna wa Maadili.
Amemtaka kwenda kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake Marehemu Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Harold Nsekela.
Aidha, Rais Magufuli amewasisitiza viongozi wote wa umma takribani 15,000 wanaotakiwa kujaza fomu za maadili, kufanya hivyo kabla ya tarehe 30 Desemba, 2020 kwa mujibu wa sheria na kwamba ndio maana amemteua Jaji Mwangesi kujaza nafasi iliyoachwa na Marehemu Nsekela ili kusiwe na visingizio.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amewatakia Watanzania wote heri ya Krismasi na Mwaka Mpya na ametaka viongozi na watumishi ambao hawana zuio la Waziri Mkuu kuruhusiwa kwenda makwao kusalimu ndugu na jamaa wakati huu wa sikukuu.