Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi ameshangazwa na kitendo cha kupotea kwa baadhi ya sampuli za Covid-19 ambazo zimekuwa zikifikishwa katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa ajili ya kufanyiwa vipimo, na kushindwa kuelewa inakuwaje sampuli hizo zinapotea na kulazimika kurudiwa, tena kwenye maabara kuu ya taifa ambayo inategemewa na maabara nyingine.
Makubi amesema hayo wakati akizungumza na uongozi wa maabara hiyo, waganga wakuu na wasimamizi wa maabara kutoka Hospital za Rufaa za Serikali na za Binafsi kutoka mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kufanya ziara katika maabara kujadili namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili maabara hiyo.
“Kwa hili la kupotea kwa sampuli kwa kweli haliwezi kuvumilika, naelekeza kwa sasa hivi nisisikie tena kuna sampuli yoyote ambayo imepotea, si vyema katika mfumo wa maabara kupoteza kwa sampuli; iwe mwiko kupotea kwa sampuli yoyote ndani ya maabara kuu ya taifa na maabara zote nchini,” amesema Prof. Makubi.
Katika hatua nyingine ameuagiza uongozi wa maabara hiyo kutoa majibu ya sampuli za Covid-19 ndani ya saa 24, badala ya saa 72 kwa hospitali zinazopeleka Sampuli hizo au kwa wananchi wanaojitokeza kupima ugonjwa huo kwa nia ya kutaka kusafiri nje ya nchi, ili kuondokana na malalamiko ambayo yamekuwa yakielekezwa kwa maabara hiyo kuwa kuna ucheleweshaji mkubwa wa majibu ya vipimo hivyo.
Amesema pamoja na kuweka mifumo mizuri katika maabara hiyo lakini bado kumekuwepo na malalamiko wanayapokea kutoka kwenye baadhi ya hospitali na hata kwa wasafiri wanaofika katika maabara hiyo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo, ucheleweshaji ambao umekuwa kero kwa wananchi hao na kamwe hautaweza kuvumiliwa.
“Tafuteni njia mtakayofanya ila hakikisheni kuanzia sasa majibu yote ya Covid-19 yanatolewa ndani ya saa 24 kwa wale wote watakaofanyiwa vipimo kwa Dar es salam na masaa 48 kwa mikoani, na lazima suala hili lisimamiwe na wasimamizi wote wa maabara zinazohusika ili kuhakikisha kero hii inaondolewa.”