Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wangi Yi anatarajiwa kuzindua Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) katika Wilaya ya Chato mkoani Geita atakapokuwa nchini kwa ziara ya siku mbili kuanzia leo Januari 7 na Januari 8, 2021.
“…. mara baada ya Mhe. Yi kuwasili hapa Chato, atazindua Chuo cha VETA cha wilaya ya Chato ambacho kimejengwa kwa fedha za watanzania,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa “sababu ya kumuomba afungue chuo hicho ni utamaduni wetu wa kumpa heshima mgeni anapokuja hapa nchini kwetu, sambamba na kutambua elimu ya mafunzo na ufundi stadi ilivyopiga hatua huko nchini China.”
Pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi amesema kuwa Serikali ya China itajenga Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) mkoani Kagera ikiwa ni namna ya kufikia lengo la Serikali kujenga VETA kila Wilaya hapa nchini.
Waziri Kabudi ameongeza kuwa shughuli nyingine zitakazofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, kuwa ni mazungumzo na Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, pamoja na kufanya mazungumzo rasmi kati yake na ujumbe wake kutoka nchini China.
Aidha, atembelea mwalo wa Chato ili kuona shughuli za uvuvi, ikizingatiwa kuwa ziwa Victoria ni ziwa la pili kwa ukubwa dunia. Pia atasaini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isaka chenye urefu wa km 341 ambapo kitagharimu kiasi cha Shilingi trilioni 3.0617
Waziri Kabudi ameogeza kuwa, Februari mwaka huu Serikali ya Tanzania inatarajia kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Guanzhou nchini China ili kukuza sekta ya utalii.
Historia ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya watu wa China ulianza mwaka 1965.