Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe amewataka wafanyakazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kufanya kazi kwa weledi ili kusaidia na kuilea sekta binafsi kwani ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
Mwambe amesema hayo alipotembelea shirika hilo jijini Dar es Salaam akiambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.
Akizungumza katika ziara hiyo Mwambie ameisisitiza TBS kujenga mazingira mazuri kwa sekta binafsi ili kuweza kuunda urafiki mzuri na kufanya biashara kuwa rahisi.
“TBS tujenge mazingira sahihi na rafiki ya kuhudumia sekta binafsi ili kuwawezesha kufanya biashara kirahisi”.
Aidha aiwataka kufanya kazi na maafisa biashara ili kufanikisha shughuli za viwango katika ngazi za halmashauri.
Naye Naibu Waziri, Exaud Kigahe amesema matumaini yao TBS ifanye kazi kwa weledi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuwawezesha wenye viwanda kuzalisha bidhaa bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yussuf Ngenya amesema wataendelea kulea sekta binafsi kwa weledi na kuwaongoza ili waweze kuzalisha bidhaa bora.