Corona: Wasafiri kutoka Tanzania na DRC wazuiwa kuingia Uingereza

0
14

Uingereza imetangaza kuzuia wasafiri kutoka Tanzania na Jamhuri ya Kidemojrasia ya Congo kuingia nchini humo kuanzia leo Ijumaa (Januari 22, 2021) ikiwa ni hatua ya kudhibiti maambukizi ya aina mpya ya virusi vya corona iliyogundulika nchini Afrika Kusini.

Katika taarifa yake, waziri wa usafiri wa Taifa hilo amesema kuwa zuio hilo halitawaathiri raia wa Uingereza, Irish au raia wa Taifa jingine wenye vibali nchini Uingereza wanaotokea kwenye nchi hizo mbili.

Grant Shapps ameeleza kuwa wanaendelea kuchukua tahadhari dhidi ya aina hiyo mpya ya virusi ikiwa ni pamoja na kuzuia baadhi ya safari na kuendesha zoezi la upimaji maambukizi kabla ya safari.

Mapema mwezi huu abiria kutoka nchi 11 za Afrika waliwekewa zuio la kuingia nchini Uingereza kwa sababu hiyo hiyo.

Kituo cha Afrika cha Kuzuia na Kupambana na Magonjwa (Africa SDC) kimesema kuwa wastani wa vifo vitokanavyo na #COVID19 barani Afrika imeongezeka kufikia asilimia 2.5, kubwa zaidi ya wastani wa dunia ambao ni asilimia 2.2.

DRC imejumuishwa katika orodha ya mataifa 21 ya Afrika ambayo wastani wa vifo vya #COVID19 ni zaidi ya asilimia 3.

Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa Tanzania ni salama na kwamba hakuna #COVID19, na hivyo kuwataka wananchi kuendelea kufanya kazi na kuzalisha zaidi ili kuyauzia chakula mataifa ambayo yameweka marufuku za kutoka nje.

Send this to a friend