Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe amesema kuwa serikali imeagiza vifaa vya kisasa nje ya nchi kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa magari yatakayokuwa yakiingia nchini.
Mwambi amesema hayo jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuhusu utaratibu mpya wa kukagua magari kuanzia Machi 2021 ambapo sasa yatakaguliwa baada ya kufika nchini, na si kwa kupitia mawakala wa nje ya nchi.
“iwahakikishie kama Serikali tumejipanga kwenye hilo, tayari tumeshaagiza vifaa maalum vya kisasa nchini Ujerumani ambavyo vitafika hivi karibuni na wataalam wetu watapatiwa mafunzo kabla ya kuanza kazi rasmi.
Kwa magari yatakayoonekana kuwa na shida yatapelekwa kwenye gereji zetu kisha yatakaguliwa tena kabla ya kupewa leseni, na vifaa hivyo vinauwezo wa kukagua gari moja kwa muda wa dakika 15,” amesema.
Amesema utaratibu wa kukagua magari yanapowasili nchini si mpya kwani umewahi kutumika mwaka 2003 na 2004.
Pia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuingia mikataba na Chuo Cha Usafirishaji (NIT) na VETA ili kuwapata watalaamu kutoka kwenye taasisi hizo ambao watapatiwa mafunzo na baadae kuajiriwa kwenye vituo vya ukaguzi wa magari hayo.
Vifaa hivyo vinatarajiwa kuingia nchini Februari 15 mwaka huu.