Rais Samia Samia Suluhu amesema uongozi wake wa Awamu ya Sita haukutokana na uchaguzi, bali umetokana na Awamu ya Tano hivyo amesema “mwelekeo wa Awamu ya Sita utakuwa ni kudumisha mema yaliyopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mema mapya, ndio maana halisi ya kaulimbiu yangu ya Kazi Iendelee.”
Amesema hayo katika kongamano la viongozi wa Dini lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma kwa lengo la kumshukuru Mungu kwa maisha ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kuliombea Taifa.
Aidha, ametaja vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita ambavyo ni kuendeleza tunu za Taifa ambazo ni kudumisha amani, umoja, mshikamano, uhuru wa Nchi na mipaka yake, kulinda Muungano pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Vipaumbele vingine ni kuendeleza jitihada za kukuza uchumi mkuu na kuutafsiri katika uchumi wa watu, kupambana na rushwa, uhujumu uchumi, wizi, ufisadi, ubadhilifu wa mali za umma, kuimarisha nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma, kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii, kuimarisha misingi ya utoaji haki, usawa, uhuru na demokrasia na kukamilisha miradi ya kimkakati na kielelezo yote pamoja na kuangalia uwezekano wa kuibua miradi mipya.
Pia, amesema serikali itaboresha mazingira ya biashara, kujenga mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali, kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuvutia mitaji kutoka nje na kuendelea kukuza uhusiano wa Kimataifa.
Rais Samia ameelezea kutofurahishwa kwake na mijadala ya mitandaoni inayomlinganisha yeye na Hayati Dkt. Magufuli na ambayo waheshimiwa wabunge wameichukua na kuizungumza Bungeni, hivyo amewasihi Wabunge kujikita katika mijadala ya msingi inayohusu Bunge la Bajeti linaloendelea na vikao vyake hivi sasa.