Serikali yamkana Cyprian Musiba, apewa onyo

0
25

SERIKALI imemuonya Mwanaharakati huru, Cyprian Musiba kuacha mara moja kufanya harakati zake kwa kuwaaminisha Watanzania kuwa Serikali inamtuma kufanya hivyo.

Onyo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe Kangi Lugola wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya kiusalama nchini.

Waziri Lugola amesema Musiba amekua akijaribu kuwaonesha na kuwaaminisha watanzania kwamba pengine Serikali imemtuma hivyo yeye kama Waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani ya Nchi anawahakikishia wananchi kwamba Serikali haiwatumi wanaharakati hao.

Amesema anafahamu kuwa wapo wanaharakati nchini wanaofanya harakati zao lakini amewaonya kuacha kufanya uwanaharakati unaopitiliza wa kuwaaminisha wananchi kuwa sisi viongozi tunabariki uwanaharakati wao.

“Nimuonye huyu Musiba kuacha kuhusisha harakati zake na Serikali au asiwaaminishe Watanzania kuwa Rais anamtuma, Serikali hatuwezi kufanya kazi kwa kuwatuma wanaharakati kutusemea.

“Kwa sababu imefikia hata wakati fulani viongozi wa Dini wanaandika waraka wakijaribu kumzungumzia huyu Musiba wanavyomuona na vitendo vyake kwamba wanadhani Serikali inabariki mambo yake. Niwahakikishie sisi hatujamtuma na tunamuonya mara moja kuacha harakati zake hizo,” Amesema Waziri Lugola.

Amesema pamoja na kwamba Serikali haimtumi Musiba na kueleza kuwa Jeshi la Polisi likibaini kuwa anaendelea kujiwasilisha katika mazingira yanayoashiria kuwajengea hofu watanzania kwamba maneno anayoyasema anatumwa na Serikali basi watamchukulia hatua kali.

“Ninarudia akiendelea kujitanabaisha kwamba anatumwa na Serikali basi tutamchukulia hatua kali sana bila kuangaliana usoni wala kuoneana huruma,” Amesema Mhe Lugola.

Amemtaka Musiba kutovuka mipaka yake na kama anafanya uwanaharakati basi asijishughulishe na mambo ya Serikali.

Send this to a friend