Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 5,001 waliokuwa wakikabiliwa na adhabu ya vifungo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho wa Miaka 57 ya Muungano wa Tanzania.
Miongoni mwa wafungwa hao 1,516 wameachiwa huru baada ya kupunguziwa robo ya adhabu zao badala ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa chini ya kifungu cha Sheria ya Magereza sura ya 58 na wafungwa 3,485 wamepunguziwa robo ya adhabu zao badala ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa chini ya kifungu cha 49 (1) cha Sheria ya Magereza sura ya 58.
Wafungwa 3,485 waliopunguziwa adhabu zao wataendelea kutumikia sehemu ya kifungo iliyobaki.
Rais Samia amewataka wafungwa wote walioachiwa huru kutumia vyema mafunzo waliyoyapata wakiwa gerezani na waungane na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa huku wakiheshimu na kuzingatia sheria.
Aidha, Rais Samia amewatakia heri Watanzania wote katika maadhimisho ya miaka 57 ya Muungano na amewataka kutumia siku hii kutafakari juhudi mbalimbali zilizofanyika katika ujenzi wa Taifa na wajibu wa kila mmoja katika kuendelea kujenga Taifa imara.
Ameahidi kuendelea kuuenzi, kuulinda na kuundeleza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa manufaa ya Watanzania wa pande zote mbili.