Dkt. Hosea: Mungu alitaka nigombee Urais TLS
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dkt. Edward Hosea amesema kuwa anaamini Mungu alimtaka kugombea nafasi hiyo ili aweze kukivusha chama hicho kutoka hapo kilipo sasa.
Akizungumza na TBC, Dkt. Hosea ameeleza kuwa awali hakuwa na mpango wa kugombea, lakini alipata shinikizo kutoka kwa watu, na baada ya kukaa na kutafakari akaona kweli chama hicho kinahitaji uongozi wake.
“… nilikuwa nafundisha Chuo Kikuu cha Iringa… nikapigiwa simu na baadhi ya watu kwamba bwana embu jaribu kugombea, nikawaambia hapana sioni sababu ya kuingia kwenye uongozi mimi, nilishastaafu.
Pressure [shinikizo] ikawa kubwa, nikaletewa fomu Iringa watu wameshajaza, mimi ni ku-sign. Sasa nikasema watu wametoa Dar es Salaam, wamejaza fomu, wacha nijaribu,” ameeleza Dkt. Hosea.
Amesema baada ya hapo alianza kuona sababu za kugombea na kwamba chama hicho kinahitaji kutolewa hapo kilipo kiende mtambuko mwingine.
“Hiyo sasa nikaanza kuiona na ikawa inanijaaa katika moyo wangu kwamba, nadhani Mungu ametaka mimi nigombee nafasi hii,” amefafanua zaidi.
Aprili 16, 2021 Dkt. Hosea alichaguliwa kuwa Rais wa TLS kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambapo miongoni mwa vipaumbele vya ni kusimamia uhuru wa mahakama, utawala wa sheria na maslahi ya mawakili/wanasheria nchini.