Dangote: Mazingira ya biashara Tanzania yamebadilika na kuimarika

0
14

Mfanyabiashara wa Nigeria, Alhaji Aliko Dangote amesema atawahimiza wafanyabiashara na wawekezaji wenzake kuwekeza Tanzania kutokana na kubadilika na kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini.

Dangote amesema hayo katika mazungumzo na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Ikulu, Dar es Salaam ambapo pia amempongeza Rais Samia kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara.

“Tutaendelea kuwekeza Tanzania ili kuzalisha ajira, mapato ya nchi na kuinua ustawi wa wananchi wa Tanzania, nadhani anahitaji kuungwa mkono katika hili na tumemuahidi kuwa tutaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa hapa Tanzania ili kuunga mkono anachokifanya, sisi tutazalisha ajira” amesema Alhaji Dangote.

Kwa upande wake, Rais Samia amempongeza Dangote kwa uwekezaji alioufanya hapa nchini na amemhakikishia kuwa Serikali itahakikisha uwekezaji wake na wawekezaji wengine unalindwa kwa manufaa ya pande zote mbili.

Dangote amewekeza hapa nchini kiasi cha Dola za Marekani milioni 770 (sawa na shilingi Trilioni 1.761) na amesema ataendelea kuwekeza katika maeneo mengine ikiwemo mpango wake wa kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea.

Send this to a friend