Tanzania ina wanawake wengi zaidi ya wanaume

0
30

Tanzania ina idadi kubwa ya wanawake kuliko wanaume ambapo hadi mwaka jana kulikuwa na wanawake zaidi ya milioni 29.4 ambao ni asilimia 51.04 ya watu wote.

Takwimu hizo zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wanawake wa Tanzania kupitia wanawake wa Mkoa wa Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Jakaya Kikwete Jijini Dodoma uliohudhuriwa na zaidi ya Wanawake 8,000.

Amesema wanawake ni jeshi kubwa ambalo linategemewa katika uchumi na ustawi wa jamii hivyo hawapaswi kubaki nyuma na badala yake watumie fursa mbalimbali zilizopo kufanya mageuzi yatakayolisaidia Taifa kusonga mbele.

Amewahimiza wanawake kote nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazowasaidia kusukuma mbele maendeleo yao na ya Taifa kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayo dhamira ya dhati ya kuwaunga mkono.

Rais Samia ametaja baadhi ya maeneo ambayo Serikali imewawezesha wanawake kiuchumi kuwa ni kuanzisha mifuko 61 ambayo imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi Trilioni 2.22 kwa wanawake Milioni 5.3 na mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 63.489 iliyowafikia wanawake 938,802.

Katika risala ya wanawake, iliyosomwa na Joyce Kashozi wanawake hao wamemshukuru Rais Samia kwa namna anavyowaamini wanawake na kuwapa nafasi nyingi za uongozi na wamemuahidi kutomuangusha.

Send this to a friend