Tanzania yatangaza siku 7 za maombolezo, kifo cha Mzee Kaunda

0
28

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza siku 7 za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Rais wa kwanza wa Zambia, Dkt. Kenneth David Kaunda, kilichotokea Juni 17, 2021 mjini Lusaka Zambia.

Katika kipindi hicho cha maombolezo, bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

Aidha, Rais Samia ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Zambia, Mhe. Edgar Chagwa Lungu, familia ya marehemu na wananchi wote wa Zambia kwa kumpoteza kiongozi wao.

Rais Samia amemtaja Mwendazake Dkt. Kaunda kuwa miongoni mwa viongozi mahiri na jasiri kuwahi kutokea barani Afrika, ambapo wakati wa uhai wake alitoa mchango mkubwa kwenye harakati za ukombozi wa Bara la Afrika kwa kushirikiana na viongozi wengine, akiwemo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Vilevile, Dkt. Kaunda alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Rais Samia amesema Tanzania itamkumbuka Kaunda kwa mchango wake katika kukuza uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa yetu mawili, ambao uliwezesha kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Mamlaka ya Reli kati ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na Bomba la Kusafirisha Mafuta (TAZAMA).

Send this to a friend