Rais Samia azungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani

0
17

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Julai 6, 2021 amezungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Blinken amempongeza Rais Samia kwa kushika hatamu ya uongozi nchini na kumhakikishia kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuleta maendeleo kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa kuzingatia vipaumbele vya nchi.

Katika mazungumzo hayo, Blinken amepongeza Rais Samia kwa hatua anazozichukua katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona nchini Tanzania na Marekani ipo tayari kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Aidha, Blinken amepongeza jitihada za Rais Samia katika kuimarisha Demokrasia nchini ikiwa ni pamoja na azma yake ya kukutana na kushirikiana na Vyama vya Siasa pamoja na kusimamia Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Pia amepongeza uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na kuahidi kuwa hali hiyo imeivutia Marekani kushawishi wawekazaji wake kuja kuwekeza nchini.

Kwa upande wake, Rais Samia ameshukuru kwa pongezi na kuahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Marekani kukuza uhusiano baina ya nchi hizi mbili katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Aidha, Rais Samia ametoa mwaliko kwa Rais wa Marekani Mhe. Joseph Biden kutembelea Tanzania ili kuzidi kuimarisha uhusino uliopo kati ya nchi hizi mbili.