Waziri Mkuu Kaasim Majaliwa ameipa siku saba za awali tume aliyoiunda kuchunguza chanzo cha moto katika soko la kimataifa la Kariakoo ili kubaini nini kimesababisha au nani kasababisha moto huo.
Ametoa kauli leo (Jumapili Julai 11, 2021) alipokuwa anaongea na wafanyabiashara na wakazi wa eneo la Kariakoo baada ya kukagua hatua zinazoendela kuchukuliwa kudhibiti moto huo, Jijini Dar es Salaam.
“Endapo itagundulika kama kuna mtu alihusika kwa namna moja au nyingine, hatua kali za kisheria zitachukuliwa moja kwa moja, kitendo cha kuungua kwa soko hili la miaka chungu mzima lazima kuwe na uchunguzi wa kina, kwanini leo lishike moto,” ameeleza Majaliwa
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wafanyabiashara katika soko hilo wawe watulivu wakati Serikali inafanya kazi yake ya kujua chanzo cha moto huo na amewahakikishia usalama wa mali zilizo ndani ya soko hilo
Waziri Mkuu pia aliwataka wafanyabiashara kutoingia ndani ya soko hilo katika kipindi hiki ambacho udhibiti unaendelea hadi pale timu zilizoundwa zitakapojiridhisha na utulivu na kufanya sensa ya watu wenye mali kuingia mmoja baada ya mwingine ili wakatoe vitu walivyoviacha
“Tunachoshukuru kule chini shimoni hakuna moto, mali zote zinalindwa, msiwe na mashaka milango yote imefungwa na makamanda wako ndani na nje wanalinda, mali zote zimehifadhiwa, msiwe na mashaka”
Kadhalika amewaahidi wafanyabiashara hao kuwa Serikali itaongea na Mabenki yaliyowakopesha wafanyabiashara waliounguliwa na mali zao kuwaongezea muda wa kulipa mikopo yao baada ya kuunguliwa.
“Tume itapata taarifa za kila mmoja mwenye mkopo rasmi kwenye taasisi za fedha ili tuzungumze nao waongeze muda waache kipindi hiki ili uweze kulipa hapo baadae utakapo kuwa umetulia, biashara imeungua naamini mabenki yatatuelewa na kuweka utaratibu mzuri.”