Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesitisha mara moja upandishwaji wa bei za gesi ya kupikia majumbani (LPG) mpaka pale itakapopokea na kupitia mapendekezo na hoja za uhalali wa kupandishwa kwa bei hizo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje imetoa agizo hilo leo baada ya kuwepo malalamiko ya wananchi juu ya kupanda kwa bei za gesi hizo bila kuwepo utaratibu rasmi.
Mbali na kuweka zuio hilo, Chibulunje ameziagiza kampuni za gesi kuwasilisha EWURA maelezo ya uhalali wa ongezeko la bei hizo mara moja kwa ajili ya uhakiki ili mamlaka hiyo iweze kuthibitisha pasi na shaka juu ya ongezeko la bei.
Ameonya kuwa, kampuni ambayo itashindwa kutekeleza agizo hilo la udhibiti itachukuliwa hatua za kisheria.
Serikali imekuwa ikipigia chapuo matumizi ya gesi majumbani ili kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ambayo inasababisha uharibifu wa mazingira, mathalini, ukataji miti.