Serikali: Kuna ziada ya sukari nchini, hatutaoa vibali vya kuagiza nje

0
21

Serikali imesema kuwa itasimamia sheria na taratibu ilizojiwekea kwenye usimamizi wa mazao mbalimbali ikiwemo miwa, hivyo haitatoa kibali kwa wafanyabiashara wa sukari badala yake kibali kitatolewa kwa wazalishaji wa ndani kama kutakuwa na uhitaji.

Imebainisha kuwa kwa sasa nchini kuna ziada ya Tani Zaidi ya 70,000 za sukari hivyo serikali haiwezi kutoa kibali chochote cha uagizaji wa sukari nje ya nchi wakati uzalishaji unaendelea nchini.

Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda amesema serikali kuendelea kutoa kibali kuagiza sukari nje ya nchi sio sahihi kwani inahatarisha uzalishaji wa sukari nchini jambo linalowakosesha ajira watanzania wengi huku likiwakosesha soko la miwa kwa wakulima ambao miwa yao huchomwa kutokana na uwezo mdogo wa viwanda vya ndani.

“Ninawaomba sana wafanyabiashara wote nchini watambue kuwa serikali inapenda sana wapate faida kwenye biashara zao lakini hii ya sukari waache tupambane ili tuweze kuzalisha ndani ya nchi,” amekaririwa Waziri Mkenda

Kauli hiyo ya Waziri wa Kilimo inajiri wakati ambapo imebainika kuwa kumekuwa na barua nyingi zinazowasilishwa Bodi ya Sukari Tanzania kwa ajili ya maombi ya kibali cha kuagiza sukari nje ya nchi.

“Mimi ndio msimamizi wa sheria kwahiyo msimuhangaishe sana Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania kwamba yeye anakataa kuwapa ruhusa ya kuingiza sukari, sheria haimruhusu na wala hainiruhusu mimi kutoa kibali hicho,” Mkenda

Sheria hiyo imeilekeza Wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa sukari iingizwe kwa utaratibu ili kuwekeza zaidi nchini, hivyo sheria hiyo haitabadilishwa kama watu wanavyofikiri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Sukari Tanzania (TSPA), Seif Ally Seif amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia uimarishaji wa viwanda nchini.

Send this to a friend