Vyombo vya habari kuwalipa wasanii kuanzia Desemba

0
13

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema kanuni zinazohusu mirabaha kwa kazi ya sanaa sio kitu kipya kwa vyombo vya habari bali ni sehemu ya utekelezaji wa haki za wasanii na wabunifu wengine kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 1999.

Dkt. Abbasi amesema hayo wakati akifungua warsha ya siku moja kwa wadau wa sanaa na habari kuhusu Kanuni za Mirabaha ya Wasanii katika vyombo vya habari vya TV, redio na mitandaoni iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

“Kanuni hizi zikianza utekelezaji Desemba mwaka huu tutaanza kugawa fedha za wasanii ambao watakuwa wamesajili kazi zao COSOTA na pia ambazo zimechezwa katika TV, redio na mitandaoni. Ni Kanuni ambazo zinakuja kugeuza kabisa mfumo wa sasa wa nchi yetu kuwa na wasanii na wabunifu maarufu lakini masikini na kuwa na wasanii maarufu lakini pia matajiri kutokana na ujira unaotokana na ubunifu wao,” amesema Dkt. Abbasi.

Kwa kauli moja wadau wote walioshiriki kikao hicho wameunga mkono kanuni hizo na kupendekeza maboresho yaendelee kufanyiwa kazi ili wasanii wanufaike na kazi zao.

Send this to a friend