Tanzania itakavyofaidika kwa Rais Samia kurekodi kipindi cha The Royal Tour

0
30

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu ameanza kurekodi kipindi maarufu cha ‘The Royal Tour’ kwa lengo la kuitangaza Tanzania hasa sekta za utalii, biashara na uwekezaji.

Kumekuwa na maswali mengi kutoka kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kuhusu kipindi hicho na mantiki au manufaa yake kwa Tanzania kiasi cha kumlazimu Rais kuacha majukumu yake mengine na kwenda kurekodi. Maswali hayo yatapatiwa majibu katika makala hii fupi kuhusu The Royal Tour.

The Royal Tour ni kipindi ambacho kimekuwa kikiruka nchini Marekani kwa miongo miwili sasa kikitumika kubadili mtazamo wa dunia kuhusu mataifa mbalimbali. Ufanyikaji wake unamhusisha kiongozi wa nchi ambaye anakuwa kama mwongoza watalii kwa kuwapitisha kwenye vivutio mbalimbali na mambo mengine ambayo anataka dunia ione vinavyopatikana nchini mwake.

Jukwaa hilo ambalo hurushwa pia Ulaya, Asia, Afrika na kwenye mitandao ya kijamii ya taasisi zenye mamilioni ya wafuasi hutoa nafasi ya kipekee kuitangaza nchi na watu wake, kwa kuionesha dunia mazuri yanayopatikana kwenye nchi husika, na kuwafanya kuielewa kupitia mwongozo wa viongozi wa nchi hizo.

Tanzania itafaidika na mengi kupitia jukwaa hilo ambapo katika utalii itaweza kuionesha dunia vivutio vya utalii vilivyopo, kuwasilisha uelewa wa juu kuhusu utamaduni wa Watanzania, lengo likiwa ni kuvutia watalii zaidi na kufikia lengo la watalii milioni 5 kwa mwaka.

Aidha, jukwaa hilo hutazamwa na watu wa daraja la juu kiuchumi hivyo litaiweka Tanzania katika ramani ya kuvutia wawekezaji linaweza kuwavutia wawekezaji kuja Tanzania kwa kuona maeneo ya kitalii wanayoweza kuwekeza, au wakavutia kutembelea Tanzania.

Tanzania itaweza kutumia kipindi hicho kufanya mawasilisho mbalimbali kwa wadau wa utalii, lakini pia kurusha kwenye kumbi za mikutano na kwenye ndege.

Shughuli ya kurekodi na kuandaa kipindi hicho inatarajiwa kukamilika Oktoba 2021 na kitaanza kuonekana Novemba mwaka huu. Utaratibu wa kipindi hicho ni kuwa kinapooneshwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani, kiongozi wa nchi husika huhudhuria ambapo pamoja na mambo mengine hupata nafasi ya kuzungumza na kujibu maswali mbalimbali.

Kabla ya Rais Samia, wengine waliowahi kufanya kipindi hicho ni Rais wa Rwanda, Paul Kagame, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa New Zealand, Hellen Clark, Mflame wa Jordan, Abdullah II na Rais wa Mexico, Filipe Calderon.

Send this to a friend