Rais Samia aja na mkakati wa kuitangaza Tanzanite

0
19

Katika hatua ya kuhakikisha kuwa wananchi na Taifa kwa ujumla wananufaika na rasilimali zilizopo, serikali imekuja na mkakati wa kuyatangaza zaidi madini ya Tanzanite dunia, ili ufahamike kuwa madini hayo adimu yanapatikana Tanzania pekee.

Mkakati huo umeelezwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na wakazi wa Mererani mkoani Manyara mara baada ya kuwasili huko ikiwa ni mwendelezo wa kurekodi vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji kupitia kipindi cha The Royal Tour.

“Huko nyuma Tanzanite yetu ilikuwa inazagaa tu. Ukienda Kenya kuna Tanzanite, Singapore Tanzanite, sijui India, inauzwa tu hovyo hovyo,” ameeleza Rais.
Ameongeza kuwa kupitia kipindi hicho ambacho kitarushwa maeneo mbalimbali duniani ikiwemo Marekani, itafahamika kuwa Tanzanite inapatikana Mererani nchini Tanzania pekee.

Aidha, ametahadharisha kuwa madini hayo yana mwisho, na kwamba ni lazima shughuli za uchimbaji na uuzaji zifanyike kwa mpangilio maalum, kwani yakiuzwa hovyo, thamani yake itashuka.

“Tukiyauza kwa mpangilio, na tukiiachia kidogo kidogo duniani, na tukifanya itokee Tanzania kwenda nje, Tanzanite yetu itapata thamani,” ameongeza.

Katika kuhakilisha madini hayo hayatoroshwi, serikali ilijenga ukuta kuzunguka eneo la machimbo, ikafunga taa na kamera za ulinzi na kuhakikisha shughuli zote za uchimbaji zinafanyika ndani ya ukuta. Hatua hizo zilichangia mapato kuongezeka kutoka milioni 165 mwaka 2016, kabla ya ukuta, hadi shilingi bilioni 2.17 mwaka 2020, baada ya ujenzi.

Send this to a friend