Mfahamu Kanali Doumbouya, kiongozi wa mapinduzi Guinea

0
33

Dunia inafahamu kuwa Rais wa Guinea, Alpha Condé amepinduliwa na jeshi kwa kile walichoeleza kuwa ni hali mbaya ya maisha yaliyoghubikwa na rushwa, ukiukwaji wa haki za binadamu na umasikini.

Lakini wengi wasichokifahamu ni kuhusu kiongozi aliyenyuma ya mapinduzi hayo ambayo yamekosolewa vikali na jumuiya za kikanda na kimataifa, zikitaka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.

Kanali Mamady Doumbouya mwenye miaka 41 ndiye kiongozi wa mapinduzi na alitangaza kutokana na sababu tajwa, jeshi halikuwa na mbadala.

“Rais yuko nasi, yuko sehemu salama,” alisema kanali huyo baada ya mapinduzi hayo na kuongeza kuwa muda wa kuifanya nchi kuwa mali ya mtu umekwisha, na kwamba wataiweka mikononi kwa wananchi.

Baada ya kukutana na mawaziri waliokuwa kwenye serikali ya Conde, amesema serikali ya umoja itaundwa karibuni na kuahidi hakutakuwa na kufukua makaburi dhidi ya maafisa waliokuwepo serikalini.

Ni mambo machache yanayofahamika kuhusu maisha ya Kanali Doumbouya, hasa kabla ya mapinduzi. Lakini anatokea katika jamii ya Malinké, sawa na Rais Conde.

Baadhi ya vyanzo vya habari vinamtaja kama kamanda mashuhuri, wakati vingine vikitilia mashaka uwezo wake.

Kanali Doumbouya ni miongoni mwa maafisa 25 wa Guinea ambao Umoja wa Ulaya (EU) imekuwa ikitishia kuwawekea vikwazo kwa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu uliotekelezwa chini ya Rais Conde.

Akitangaza mapinduzi hayo Jumapili alimnukuu Jerry Rawlings wa Ghana aliyetwaa madaraka mwaka 1979 kuwa, watu wanaponynyaswa na viongozi wa juu, ni jukumu la jeshi kuwapa watu uhuru wao.

Katika miaka 15 aliyokaa jeshini ametumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo Afghanistan, Ivory Coast, Djibouti, Afrika ya Kati, Israel, Cyprus, Uingereza na Guinea.

Imeelezwa kuwa amehitimu vizuri mafunzo maalum ya ulinzi (operational protection specialist training) kutoka Irsael (International Security Academy) pamoja na mfunzo mengine ya jeshi kutoka Senegal, Gabon na Ufaransa.

Baada ya kutumika katika jeshi la Ufaransa kwa miaka kadhaa aliombwa na Rais Conde kurejea Guinea kuongoza kikundi maalum ndani ya jeshi (Special Forces Group (GFS)) mwaka 2018.

Alikaa eneo la Forecariah, Magharibi mwa Guinea, ambapo alifanya kazi chini ya bureau of territorial surveillance (DST) na ujasusi (general intelligence services).

Ni wazi kuwa Rai Conde hakujua kwamba anajichimbia shimo la kisiasa wakati alipomwomba kiongozi huyo kurejea nchini humo.

Send this to a friend