Sababu za Tanzania kuifanya bangi kosa la jinai
Bunge la Tanzania jana limepitisha muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali ikiwemo kufanya kuwa kosa la jinai kitendo cha kukutwa na au kutumia kiwango kidogo cha dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi.
Hatua hiyo imetokana na sheria iliyopo sasa kuzuia kitendo hicho, lakini haitamki kama mtu kutumia au kukutwa nayo ni kosa jinai.
Tanzania yakanusha kuruhusu matumizi ya bangi
Uamuzi huo umeibua maswali mengi sana kwenye mitandao ya kijamii, hasa ikizingatiwa baadhi ya mataifa mbalimbali dunia yameidhinisha kilimo cha bangi kwa ajili ya shughuli za kitabibu au kusafirisha nje ya nchi, hivyo inaonekana kuwa Tanzania imefungia fursa.
Huenda serikali imechukua uamuzi huo kutokana na madhara ya kutumia mmea huo ambayo pengine wananchi hawajui. Mara nyingi bangi imekuwa ni kati ya dawa ya awali kutumiwa, ambapo watumiaji wengi huanza matumizi wakiwa na umri mdogo hivyo kuwa katika hatari zaidi kiafya, kijamii na kiuchumi. Hivyo, bangi hutumika kama njia ya kuingia katika matumizi ya dawa nyingine za kulevya.
Haya ni baadhi ya madhara ya bangi kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA):
- Bangi huamsha magonjwa ya akili hususani, ‘depression’, ‘anxiety’ ‘psychosis’na ‘schizophrenia.’
- Moshi wa bangi huzalisha lami na kemikali mbalimbali ambazo zinaweza kusababisha kansa ya mapafu.
- Bangi huathiri mifumo ya fahamu na kumfanya mtumiaji awe kwenye hali ya njozi ambapo ataona na kusikia vitu tofauti na uhalisia. Hali hii inachangia kupunguza stamina ya mtumiaji na kusababisha ajali, uharibifu wa mali pamoja na kushusha ufanisi wa kazi.
- Baadhi ya watumiaji hupata wasiwasi mkubwa mara wavutapo na kuwahisi vibaya watu wanaowazunguka kuwa wanataka kuwadhuru au kuhisi wanajua kuwa wamevuta bangi. Wasiwasi huweza kumfanya mtumiaji amshambulie mtu na kumdhuru bila hatia.
- Mara baada ya kutumia bangi mapigo ya moyo huongezeka na mishipa ya damu kupanuka na hata kusababisha kiharusi.
- Uvutaji wa bangi huweza kusababisha kikohozi sugu, kukosa pumzi, vidonda vya koo na pumu
- Mtumiaji wa bangi hukosa mwamko wa maendeleo akijihisi ni mwenye maendeleo makubwa wakati anaishi maisha duni kabisa.
- Matumizi ya bangi huchochea mmomonyoko wa maadili kutokana na ongezeko la vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi, utapeli na ukatili wa kijinsia katika jamii.
- Bangi husababisha utegemezi, huvuruga mahusiano ya kifamilia pamoja na upotevu wa ajira kwa mtumiaji. Matokeo ya kuvurugika mahusiano ni pamoja na kuwepo kwa migogoro isiyoisha, kutelekeza wenza na watoto, kuvunjika kwa ndoa, kutokuwa na ajira, ongezeko la watoto wa mitaani na biashara ya ngono.