Sirro: Jeshi la Polisi kukagua yanayofundishwa nyumba za ibada

0
28

Jeshi la Polisi Tanzania limesema kuwa lintakuwa likipita katika nyumba za ibada kukagua mafunzo wanayofundishwa watoto katika madrasa na shule za Jumapili (Sunday schools) kufahamu aina ya mafundisho yanayotolewa.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro ameeleza hayo wakati akizungumzia ziara yake ya siku nne nchini Rwanda na kusema wamejifunza hilo kutoka huko, hivyo ni vyema wapite kwenye maneno hayo kujua malengo ya mafunzo yanayotolewa.

“Tumeona wenzetu hizi shule za dini, kwa mfano haya Madrasa, kwa mfano hizo Sunday schools kuna kikosi maalum kuona mafunzo yanayofundishwa. Je! Mafunzo yale yanatolewa kwa ajili ya uzalendo, au ni mafunzo yanayotolewa kwa ajili ya kuharibu nchi,” amesema Sirro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Sirro ameeleza utaratibu huo ni mzuri na kwamba watawashirikisha viongozi wa dini na timu ya kupambana na makosa ya kigaidi kuona namna ya kupitia mafunzo yanayofundishwa kwenye shule za dini na shule za elimu dunia, hadi ngazi ya vyuo vikuu, kuona kama mafunzo yanawajenga au yanawabomoa vijana.

Aidha, ameitaka jamii kutoa taarifa endapo itabaini kuna mtu ana tabia au mwenendo kinyume na jamii husika, na kwamba sio lazima mhusika afungwe, bali wanaweza kumsaidia kuwa mtu mwema na akaendelea na shughuli zake.

Send this to a friend