Spika wa Bunge wa Tanzania, Job Ndugai amemwagiza Waziri wa Nishati, January Makamba kuhakikisha anasimamia vizuri wizara hiyo na kutatua changamoto nyingi za nishati zinazowakumba wananchi ikiwemo bei ya mafuta, kukatika kwa umeme na kukamilishwa kwa miradi ya kimkakati.
Ndugai ametoa rai hiyo wakati akizungumza baada ya kuapishwa kwa mawaziri wapya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Septemba 12 mwaka huu ikiwa ni mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri.
“Tuna matatizo makubwa sana kwenye petroli na dizeli na jamii zake zote. Ni matarajio yetu kwamba utakwenda kuliangalia hilo na bei ya petroli isipande kama inavyokwenda, tuangalie mbinu mbadala nini tunaweza kufanya kuwa na ‘stability’ [uimara] kwenye eneo hilo,” amesema Ndugai.
Mbali na nishati hiyo amemtaka kuendeleza juhudi zake ambazo alizianza akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati za kurekebisha mikataba ya nishati kutoka kwenye mikataba mibovu ambayo nchi ilikuwa imeingia na kuisababishia asara kubwa. Pia,Ndugai ametaja kero ya kukatika umeme mara kwa mara wakati mwingine hadi mara 30 kwa siku, na kwamba ni jambo linalokera, hivyo ni lazima limalizike.
Wakati huo huo, Spika Ndugai amemtaka Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Ashatu Kijaji kujikita katika kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kwamba itarahisisha utoaji huduma kwa wananchi na pia kupunguza vitendo vya rushwa.