Serikali imekanusha taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa imewataka wafanyabiashara wote wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni walionyang’anywa vifaa vya, kwenda kuvichukua.
Wizara ya Fedha na Mipango imesema kuwa habari hiyo imepotosha maelezo yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Masauni bungenii, na kwamba yeye alisema baada ya hatua hizo, wafanyabiashara hao waliitwa kufanya majadiliano na wizara husika na baada ya kumalizika waliotakiwa kulipa walipe, na waliotakiwa kwenda kuchukua vifaa vyao waende baada ya kukamilisha taratibu.
“Nitoe wito kama kuna wafanyabiashara ambao hawajachukua vifaa vyao na wanastahili kwenda kuvichukua, waende wakavichukue kwani hakuna sababu ya serikali kukaa na mali ya mtu bila sababu ya msingi,” alisema Masauni bungeni.
Wizara imesisitiza kuwa katika majibu hayo Masauni hakusema wafanyabiashara wote, bali ni wale tu wanaoona wanastahili kuchukua, ambao wametimiza vigezo na masharti.