Waziri Mkuu aagiza kupigwa marufuku kamba za plastiki

0
23

Wizara ya Kilimo imesema inakamilisha sera itakayozuia uzalishaji na matumizi ya kamba za plastiki ikiwa ni mkakati wa kukuza uzalishaji na matumizi ya kamba za katani.

Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe katika mkutano wa wadau wa katani uliofanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Katika hotuba yake ambayo amesema imeandaliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Bashe ameitaka kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kudhibiti kuanzia uzalishaji hadi uingizwaji sokoni wa kamba za plastiki.

Aidha, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeagizwa kuandaa kanuni za kuzuia matumizi ya plastiki kutokana na kuwa hatari kwa mazingira na hazichangii serikali mapato.

Moja ya changamoto kubwa zinazokabili uzalishaji wa katani nchini mafuruko ya kamba za plastiki sokoni ambazo zinaonekana ni imara zaidi kuliko za katani, licha ya kwamba ni hatari kwa mazingira.

Akiwa mkoani Tanga Januari mwaka huu Waziri Mkuu alielezwa kwamba kamba hizo zinazalishwa na viwanda ambavyo havijulikani vilipo, na zinauzwa bila kuidhinishwa na TBS, hivyo wazalishaji hawalipi kodi.

Send this to a friend