Kikwete: Rais Samia anaongoza nchi vizuri

0
41

Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete amewasihi Watanzania kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi, huku akuongeza kuwa hadi sasa anaiongoza nchi vizuri na kuwapa wananchi matumaini.

Dkt. Kikwete ametoa rai hiyo Septemba 14 mwaka huu akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze utakaogharimu shilingi bilioni 1.2 huko Msoga. Ujenzi huo unafadhiliwa na Shirika la Abbott linalojihusisha na masuala ya afya kutoka Marekani.

“Tuendelee kumuunga mkono Rais wetu. Anayo dhamana kubwa, si kazi rahisi, ina mawimbi mengi. Wakati mwingine kwenye kazi ile unapata siku za furaha ni kidogo kuliko siku za maudhi,” amesema Kikwete na uongeza kuwa “mpaka sasa anaongoza nchi vizuri na kwamba changamoto hazikosekani.”

Ameeleza kuwa Rais Samia atapata moyo zaidi atakapoona Watanzania wanaendelea kumuunga mkono, kumwonesha kwamba wako pamoja naye.

“Ukiwa pamoja na wenzako unapata moyo wa kukabiliana na changamoto kubwa zilizopo kwenye ofisi ile,” amesisitiza Dkt. Kikwete.

Ni miezi sita sasa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aapishwe kuwa Rais wa Tanzania ambapo aliapishwa Machi 19 mwaka huu, siku mbili baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

Send this to a friend