Sudan Kusini imeomba kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo yake na pia kununua chakula kutoka Tanzania.
Hayo yameelezwa na Mjumbe Maalum wa Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit, Balozi Albino Ayuel Aboug, Ikulu jijini Dar es Salaam alipowasilisha ujumbe kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Balozi Aboug amesema pindi reli ya kisasa (SGR) itakapokamilika nchi yake ingependa kusafirishia bidhaa zake kupitia reli hiyo, hatua ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo.
Pia, amesema Sudan Kusini bado inahitaji kupata walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili kuanzia ngazi ya shule za msingi kutoka nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Rais Samia amemuhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Sudan Kusini kutumia Bandari ya Dar es Salaam katika kukuza uchumi wa nchi zote mbili.