Benki Dunia (WB) imesema ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika ununuzi, usafirishaji na utoaji elimu ya UVIKO 19 kwa jamii ili kutoa muamko kwa wananchi kujitokeza kupata chanjo.
Aidha, benki hiyo imeeleza dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania katika kuwajengea uwezo wanawake kiuchumi kuanzia wanapozaliwa, kimasomo na katika afya.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Hafez Ghanem alipofika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika mazungumzo hayo, Rais Samia amemueleza Dkt. Ghanem vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita ambavyo ni kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu na afya pamoja na ujenzi wa miradi ya kimkakati.
Aidha, Rais Samia amemueleza kuwa kwa sasa Serikali inapitia sera zake za kodi kwa majadiliano na wadau ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji katika kuimarisha sekta binafsi ili iweze kushindana na kuchangia ajira nchini.
Rais Samia pia amezungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali kuweka taarifa na kuongeza ufanisi katika makusanyo kupitia matumizi ya TEHAMA.